NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 99

1 Bwana anatawala, mataifa na yatetemeke; anakalia kiti cha enzi katikati ya makerubi, dunia na itikisike.

2 Bwana ni mkuu katika Sayuni; ametukuzwa juu ya mataifa yote.

3 Wanalisifu jina lako ambalo ni kuu na la kuogopwa: yeye ni mtakatifu!

4 Mfalme ni mwenye nguvu na hupenda haki, wewe umethibitisha adili; katika Yakobo umefanya yaliyo haki na sawa.

5 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu, na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake; yeye ni mtakatifu.

6 Mose na Aroni walikuwa miongoni mwa makuhani wake, Samweli alikuwa miongoni mwa walioliitia jina lake; walimwita Bwana, naye aliwajibu.

7 Alizungumza nao kutoka nguzo ya wingu; walizishika sheria zake na amri alizowapa.

8 Ee Bwana, wetu, ndiwe uliyewajibu, kwa Israeli ulikuwa Mungu mwenye kusamehe, ingawa uliadhibu matendo yao mabaya.

9 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu, mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu, kwa maana Bwana Mungu wetu ni mtakatifu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0