NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 96

1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya; mwimbieni Bwana dunia yote.

2 Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.

3 Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa, matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.

4 Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.

5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini Bwana aliziumba mbingu.

6 Fahari na enzi viko mbele yake; nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.

7 Mpeni Bwana, enyi jamaa za mataifa, mpeni Bwana utukufu na nguvu.

8 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; leteni sadaka na mje katika nyua zake.

9 Mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake; dunia yote na itetemeke mbele zake.

10 Katikati ya mataifa semeni, “Bwana anatawala.” Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa; atawahukumu watu kwa uadilifu.

11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake;

12 mashamba na yashangilie, pamoja na vyote vilivyomo ndani yake. Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;

13 itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja, anakuja kuihukumu dunia. Ataihukumu dunia kwa haki, na mataifa katika kweli yake.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0