NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 75

1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Zaburi ya Asafu. Wimbo. Ee Mungu, tunakushukuru, tunakushukuru wewe, kwa kuwa jina lako li karibu; watu husimulia matendo yako ya ajabu.

2 Unasema, “Ninachagua wakati maalum; ni mimi nihukumuye kwa haki.

3 Wakati dunia na watu wake wote inapotetemeka, ni mimi ninayezishikilia nguzo zake imara.

4 Kwa wale wenye majivuno ninasema, ‘Msijisifu tena,’ kwa wale waovu, ‘Msiinue pembe zenu.

5 Msiinue pembe zenu dhidi ya mbingu; msiseme kwa shingo zilizonyooshwa.’ ”

6 Hakuna yeyote atokaye mashariki wala magharibi au kutoka jangwani awezaye kumkweza mwanadamu.

7 Bali Mungu ndiye ahukumuye: Humshusha huyu na kumkweza mwingine.

8 Mkononi mwa Bwana kuna kikombe kilichojaa mvinyo unaotoka povu uliochanganywa na vikolezo; huumimina, nao waovu wote wa dunia hunywa mpaka tone la mwisho.

9 Bali mimi, nitatangaza hili milele; nitaimba sifa kwa Mungu wa Yakobo.

10 Nitazikatilia mbali pembe za waovu wote, bali pembe za wenye haki zitainuliwa juu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0