NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 64

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu, uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui.

2 Unifiche kutokana na shauri la siri la waovu, kutokana na zile kelele za kundi la watenda mabaya.

3 Wananoa ndimi zao kama panga na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha.

4 Hurusha mishale kutoka kwenye mavizio kwa mtu asiye na hatia, humrushia ghafula bila woga.

5 Kila mmoja humtia moyo mwenzake katika mipango mibaya; huzungumza juu ya kuficha mitego yao, nao husema, “Ni nani ataiona?”

6 Hufanya shauri baya la dhuluma na kusema, “Tumebuni mpango mkamilifu!” Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.

7 Bali Mungu atawapiga kwa mishale, nao ghafula wataangushwa.

8 Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao na kuwaleta kwenye maangamizi; wote wawaonao watatikisa vichwa vyao kwa dharau.

9 Wanadamu wote wataogopa, watatangaza kazi za Mungu na kutafakari yale aliyoyatenda.

10 Wenye haki na wafurahi katika Bwana, na wakimbilie kwake; wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0