NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 6

1 Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako, wala usiniadhibu katika ghadhabu yako.

2 Unirehemu Bwana, kwa maana nimedhoofika; Ee Bwana, uniponye, kwa maana mifupa yangu ina maumivu makali.

3 Nafsi yangu ina uchungu mwingi. Mpaka lini, Ee Bwana, mpaka lini?

4 Geuka Ee Bwana, unikomboe, uniokoe kwa sababu ya fadhili zako.

5 Hakuna mtu anayekukumbuka akiwa amekufa. Ni nani awezaye kukusifu akiwa kuzimu?

6 Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni; usiku kucha nafurikisha kitanda changu kwa machozi; nimelowesha viti vyangu vya fahari kwa machozi.

7 Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika, yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote.

8 Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya, kwa maana Bwana amesikia kulia kwangu.

9 Bwana amesikia kilio changu kwa huruma, Bwana amekubali sala yangu.

10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, watarudi nyuma kwa aibu ya ghafula.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0