NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 53

1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi. Utenzi wa Daudi. Mpumbavu anasema moyoni mwake, “Hakuna Mungu.” Wameharibika, na njia zao ni za uovu kabisa, hakuna hata mmoja atendaye mema.

2 Mungu anawachungulia wanadamu chini kutoka mbinguni aone kama wako wenye akili, wowote wanaomtafuta Mungu.

3 Kila mmoja amegeukia mbali, wameharibika wote pamoja, hakuna atendaye mema. Naam, hakuna hata mmoja!

4 Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza: wale ambao huwala watu wangu kama watu walavyo mkate, hao ambao hawamwiti Mungu?

5 Hapo waliingiwa na hofu kuu, ambapo hapakuwa cha kutetemesha. Mungu alitawanya mifupa ya wale waliokushambulia; uliwaaibisha, kwa sababu Mungu aliwadharau.

6 Laiti wokovu wa Israeli ungalikuja kutoka Sayuni! Wakati Mungu arejeshapo wafungwa wa watu wake, Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0