NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 52

1 Kwa mwimbishaji. Utenzi wa Daudi. Baada ya Doegi, Mwedomu kumwendea Sauli na kumjulisha kuwa: “Daudi amekwenda nyumbani kwa Ahimeleki.” Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya? Kwa nini unajivuna mchana kutwa, wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?

2 Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi. Ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila.

3 Unapenda mabaya kuliko mema, uongo kuliko kusema kweli.

4 Unapenda kila neno lenye kudhuru, ewe ulimi wenye hila!

5 Hakika Mungu atakushusha chini kwa maangamizi ya milele: atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu kutoka hema yako, atakungʼoa kutoka nchi ya walio hai.

6 Wenye haki wataona na kuogopa, watamcheka, wakisema,

7 “Huyu ni yule mtu ambaye hakumfanya Mungu kuwa ngome yake, bali alitumainia wingi wa utajiri wake, na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”

8 Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni unaostawi katika nyumba ya Mungu, nautegemea upendo wa Mungu usiokoma milele na milele.

9 Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda, nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema. Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0