NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 47

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Pigeni makofi, enyi mataifa yote, mpigieni Mungu kelele za shangwe!

2 Jinsi gani alivyo wa kutisha, Bwana Aliye Juu Sana, Mfalme mkuu juu ya dunia yote!

3 Ametiisha mataifa chini yetu watu wengi chini ya miguu yetu.

4 Alituchagulia urithi wetu, fahari ya Yakobo, aliyempenda.

5 Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti za tarumbeta.

6 Mwimbieni Mungu sifa, imbeni sifa, mwimbieni sifa Mfalme wetu, imbeni sifa.

7 Kwa kuwa Mungu ni mfalme wa dunia yote, mwimbieni zaburi za sifa.

8 Mungu anatawala juu ya mataifa, Mungu ameketi juu ya kiti chake cha enzi kitakatifu.

9 Wakuu wa mataifa wanakusanyika kama watu wa Mungu wa Abrahamu, kwa kuwa wafalme wa dunia ni mali ya Mungu; yeye ametukuka sana.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0