NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 46

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi. Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.

3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka, milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.

4 Kuna mto ambao vijito vyake vinaufurahisha mji wa Mungu, mahali patakatifu ambako Aliye Juu Sana anaishi.

5 Mungu yuko katikati yake, hautaanguka, Mungu atausaidia asubuhi na mapema.

6 Mataifa yanafanya ghasia, falme zinaanguka, Yeye huinua sauti yake, dunia ikayeyuka.

7 Bwana Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

8 Njooni mkaone kazi za Bwana jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.

9 Anakomesha vita hata miisho ya dunia, anakata upinde na kuvunjavunja mkuki, anateketeza ngao kwa moto.

10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu; nitatukuzwa katikati ya mataifa, nitatukuzwa katika dunia.”

11 Bwana Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi; Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0