NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 29

1 Zaburi ya Daudi. Mpeni Bwana, enyi mashujaa, mpeni Bwana utukufu na nguvu.

2 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.

3 Sauti ya Bwana iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, Bwana hupiga radi juu ya maji makuu.

4 Sauti ya Bwana ina nguvu; sauti ya Bwana ni tukufu.

5 Sauti ya Bwana huvunja mierezi; Bwana huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni.

6 Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni urukaruke kama mwana nyati.

7 Sauti ya Bwana hupiga kwa miali ya umeme wa radi.

8 Sauti ya Bwana hutikisa jangwa; Bwana hutikisa Jangwa la Kadeshi.

9 Sauti ya Bwana huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!”

10 Bwana huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; Bwana ametawazwa kuwa Mfalme milele.

11 Bwana huwapa watu wake nguvu; Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0