NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 28

1 Zaburi ya Daudi. Ninakuita wewe, Ee Bwana, Mwamba wangu; usiwe kwangu kama kiziwi. Kwa sababu ukinyamaza nitafanana na walioshuka shimoni.

2 Sikia kilio changu unihurumie ninapokuita kwa ajili ya msaada, niinuapo mikono yangu kuelekea Patakatifu pa Patakatifu pako.

3 Usiniburute pamoja na waovu, pamoja na hao watendao mabaya, ambao huzungumza na jirani zao maneno mazuri, lakini mioyoni mwao wameficha chuki.

4 Walipe sawasawa na matendo yao, sawasawa na matendo yao maovu; walipe sawasawa na kazi za mikono yao, uwalipe wanavyostahili.

5 Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Bwana, na yale ambayo mikono yake imetenda, atawabomoa na kamwe hatawajenga tena.

6 Bwana asifiwe, kwa maana amesikia kilio changu nikimwomba anihurumie.

7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini yeye, nami nimesaidiwa. Moyo wangu unarukaruka kwa furaha nami nitamshukuru kwa wimbo.

8 Bwana ni nguvu ya watu wake, ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.

9 Waokoe watu wako na uubariki urithi wako; uwe mchungaji wao na uwabebe milele.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0