NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 20

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Bwana na akujibu unapokuwa katika dhiki, jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako.

2 Na akutumie msaada kutoka patakatifu na akupatie msaada kutoka Sayuni.

3 Na azikumbuke dhabihu zako zote, na azikubali sadaka zako za kuteketezwa.

4 Na akujalie haja ya moyo wako, na aifanikishe mipango yako yote.

5 Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda, tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu. Bwana na akupe haja zako zote.

6 Sasa nafahamu kuwa Bwana humwokoa mpakwa mafuta wake, humjibu kutoka mbingu yake takatifu kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume.

7 Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi, bali sisi tutalitumainia jina la Bwana, Mungu wetu.

8 Wao wameshushwa chini na kuanguka, bali sisi tunainuka na kusimama imara.

9 Ee Bwana, mwokoe mfalme! Tujibu tunapokuita!

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0