NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 16

1 Utenzi wa Daudi. Ee Mungu, uniweke salama, kwa maana kwako nimekimbilia.

2 Nilimwambia Bwana, “Wewe ndiwe Bwana wangu; pasipo wewe sina jambo jema.”

3 Kwa habari ya watakatifu walioko duniani, ndio walio wa fahari ambao ninapendezwa nao.

4 Huzuni itaongezeka kwa wale wanaokimbilia miungu mingine. Sitazimimina sadaka zao za damu au kutaja majina yao midomoni mwangu.

5 Bwana umeniwekea fungu langu na kikombe changu; umeyafanya mambo yangu yote yawe salama.

6 Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri, hakika nimepata urithi mzuri.

7 Nitamsifu Bwana ambaye hunishauri, hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha.

8 Nimemweka Bwana mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika.

9 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika salama,

10 kwa maana hutaniacha kaburini, wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu.

11 Umenijulisha njia ya uzima; utanijaza na furaha mbele zako, pamoja na furaha za milele katika mkono wako wa kuume.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0