NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 142

1 Utenzi wa Daudi. Alipokuwa pangoni. Maombi. Namlilia Bwana kwa sauti, nainua sauti yangu kwa Bwana anihurumie.

2 Namimina malalamiko yangu mbele zake, mbele zake naeleza shida zangu.

3 Wakati roho yangu inapozimia ndani yangu, wewe ndiwe unajua njia zangu. Katika njia ninayopita watu wameniwekea mtego.

4 Tazama kuume kwangu na uone, hakuna hata mmoja anayejihusisha nami. Sina kimbilio, hakuna anayejali maisha yangu.

5 Ee Bwana, nakulilia wewe, nasema, “Wewe ni kimbilio langu, fungu langu katika nchi ya walio hai.”

6 Sikiliza kilio changu, kwa sababu mimi ni mhitaji sana; niokoe na wale wanaonifuatilia, kwa kuwa wamenizidi nguvu.

7 Nifungue kutoka kifungo changu, ili niweze kulisifu jina lako. Ndipo wenye haki watanizunguka, kwa sababu ya wema wako kwangu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0