NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 138

1 Zaburi ya Daudi. Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote, mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako.

2 Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu, nami nitalisifu jina lako kwa ajili ya upendo wako na uaminifu, kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako juu ya vitu vyote.

3 Nilipoita, ulinijibu; ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari.

4 Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Bwana, wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako.

5 Wao na waimbe kuhusu njia za Bwana, kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu.

6 Ingawa Bwana yuko juu, humwangalia mnyonge, bali mwenye kiburi yeye anamjua kutokea mbali.

7 Nijapopita katikati ya shida, wewe unayahifadhi maisha yangu, unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, kwa mkono wako wa kuume unaniokoa.

8 Bwana atatimiza kusudi lake kwangu, Ee Bwana, upendo wako wadumu milele: usiziache kazi za mikono yako.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0