NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 12

1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. Bwana tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka; waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu.

2 Kila mmoja humwambia jirani yake uongo; midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu.

3 Bwana na akatilie mbali midomo yote ya hila na kila ulimi uliojaa majivuno,

4 ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda; midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?”

5 “Kwa sababu ya uonevu wa wanyonge na kulia kwa uchungu kwa wahitaji, nitainuka sasa,” asema Bwana. “Nitawalinda kutokana na wale wenye nia mbaya juu yao.”

6 Maneno ya Bwana ni safi, kama fedha iliyosafishwa katika tanuru, iliyosafishwa mara saba.

7 Ee Bwana, utatuweka salama na kutulinda na kizazi hiki milele.

8 Watu waovu huenda wakiringa kila mahali wakati ambapo yule aliye mbaya sana ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0