NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 113

1 Msifuni Bwana. Enyi watumishi wa Bwana msifuni, lisifuni jina la Bwana.

2 Jina la Bwana na lisifiwe, sasa na hata milele.

3 Kuanzia mawio ya jua hadi machweo yake, jina la Bwana linapaswa kusifiwa.

4 Bwana ametukuka juu ya mataifa yote, utukufu wake juu ya mbingu.

5 Ni nani aliye kama Bwana Mungu wetu, Yeye ambaye ameketi juu kwenye kiti cha enzi,

6 ambaye huinama atazame chini aone mbingu na nchi?

7 Huwainua maskini kutoka mavumbini, na kuwanyanyua wahitaji kutoka kwenye jalala,

8 huwaketisha pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake.

9 Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake, akiwa mama watoto mwenye furaha. Msifuni Bwana.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0