NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 111

1 Msifuni Bwana. Nitamtukuza Bwana kwa moyo wangu wote, katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko.

2 Kazi za Bwana ni kuu, wote wanaopendezwa nazo huzitafakari.

3 Kazi zake zimejaa fahari na utukufu, haki yake hudumu daima.

4 Amefanya maajabu yake yakumbukwe, Bwana ni mwenye neema na huruma.

5 Huwapa chakula wale wanaomcha, hulikumbuka agano lake milele.

6 Amewaonyesha watu wake uwezo wa kazi zake, akiwapa nchi za mataifa mengine.

7 Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki, mausia yake yote ni ya kuaminika.

8 Zinadumu milele na milele, zikifanyika kwa uaminifu na unyofu.

9 Aliwapa watu wake ukombozi, aliamuru agano lake milele: jina lake ni takatifu na la kuogopwa.

10 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima, wote wanaozifuata amri zake wana busara. Sifa zake zadumu milele.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0