NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 110

1 Zaburi ya Daudi. Bwana amwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, mpaka nitakapowafanya adui zako kuwa mahali pa kuweka miguu yako.”

2 Bwana ataeneza fimbo yako ya utawala yenye nguvu kutoka Sayuni; utatawala katikati ya adui zako.

3 Askari wako watajitolea kwa hiari katika siku yako ya vita. Ukiwa umevikwa fahari takatifu, kutoka tumbo la mapambazuko utapokea umande wa ujana wako.

4 Bwana ameapa, naye hatabadilisha mawazo yake: “Wewe ni kuhani milele, kwa mfano wa Melkizedeki.”

5 Bwana yuko mkono wako wa kuume, atawaponda wafalme siku ya ghadhabu yake.

6 Atawahukumu mataifa, akilundika mizoga na kuwaponda watawala wa dunia nzima.

7 Atakunywa maji katika kijito kando ya njia, kwa hiyo atainua kichwa chake juu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0