NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 11

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Kwa Bwana ninakimbilia, unawezaje basi kuniambia: “Ruka kama ndege kwenye mlima wako.

2 Hebu tazama, waovu wanapinda pinde zao, huweka mishale kwenye uzi wake, wakiwa gizani ili kuwapiga wale wanyofu wa moyo.

3 Wakati misingi imeharibiwa, mwenye haki anaweza kufanya nini?”

4 Bwana yuko ndani ya Hekalu lake takatifu; Bwana yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni. Huwaangalia wana wa watu, macho yake yanawajaribu.

5 Bwana huwajaribu wenye haki, lakini waovu na wanaopenda jeuri, nafsi yake huwachukia.

6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali na kiberiti kinachowaka, upepo wenye joto kali ndio fungu lao.

7 Kwa kuwa Bwana ni mwenye haki, yeye hupenda haki. Wanyofu watauona uso wake.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0