NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Zaburi 1

1 Heri mtu yule ambaye haendi katika shauri la watu waovu, wala hasimami katika njia ya wenye dhambi, au kuketi katika baraza la wenye mizaha.

2 Bali huifurahia sheria ya Bwana, naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana.

3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito vya maji, ambao huzaa matunda kwa majira yake na majani yake hayanyauki. Lolote afanyalo hufanikiwa.

4 Sivyo walivyo waovu! Wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.

5 Kwa hiyo waovu hawatastahimili hukumu, wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki.

6 Kwa maana Bwana huziangalia njia za mwenye haki, bali njia ya waovu itaangamia.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0