NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Yona 2

1 Akiwa ndani ya tumbo la nyangumi, Yona alimwomba Bwana Mungu wake.

2 Akasema: “Katika shida yangu nalimwita Bwana, naye akanijibu. Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada, nawe ukasikiliza kilio changu.

3 Ulinitupa kwenye kilindi, ndani kabisa ya moyo wa bahari, mikondo ya maji ilinizunguka, mawimbi yako yote na viwimbi vilipita juu yangu.

4 Nikasema, ‘Nimefukuziwa mbali na uso wako, hata hivyo nitatazama tena kuelekea Hekalu lako takatifu.’

5 Maji yaliyonimeza yalinitisha, kilindi kilinizunguka; mwani ulijisokota kichwani pangu.

6 Nilizama chini sana mpaka pande za mwisho za milima, makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele. Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni, Ee Bwana Mungu wangu.

7 “Wakati uhai wangu ulipokuwa unatoka, nilikukumbuka wewe, Bwana, nayo maombi yangu yalikufikia wewe, katika Hekalu lako takatifu.

8 “Wale watu wanaongʼangʼana na sanamu zisizofaa hupoteza neema ile ambayo ingekuwa yao.

9 Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani, nitakutolea dhabihu. Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza. Wokovu watoka kwa Bwana.”

10 Basi Bwana akamwamuru yule nyangumi, naye akamtapika Yona katika nchi kavu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0