NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Yeremia 47

1 Hili ndilo neno la Bwana lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaishambulia Gaza:

2 Hili ndilo asemalo Bwana: “Tazama jinsi maji yanavyoinuka huko kaskazini, yatakuwa mafuriko yenye nguvu sana. Yataifurikia nchi na vitu vyote vilivyomo ndani yake, miji na wale waishio ndani yake. Watu watapiga kelele; wote waishio katika nchi wataomboleza

3 kwa sauti ya kwato za farasi waendao mbio, kwa sauti ya magari ya adui na mngurumo wa magurudumu yake. Baba hawatageuka kuwasaidia watoto wao, mikono yao italegea.

4 Kwa maana siku imewadia kuwaangamiza Wafilisti wote na kuwakatilia mbali walionusurika wote ambao wangeweza kusaidia Tiro na Sidoni. Bwana anakaribia kuwaangamiza Wafilisti, mabaki toka pwani za Kaftori.

5 Gaza atanyoa kichwa chake katika kuomboleza, Ashkeloni atanyamazishwa. Enyi mabaki kwenye tambarare, mtajikatakata wenyewe mpaka lini?

6 “Mnalia, ‘Aa, upanga wa Bwana, utaendelea mpaka lini ndipo upumzike? Rudi ndani ya ala yako; acha na utulie.’

7 Lakini upanga utatuliaje wakati Bwana ameuamuru, wakati ameuagiza kuishambulia Ashkeloni pamoja na pwani yake?”

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0