NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Isaya 35

1 Jangwa na nchi kame vitafurahi; nyika itashangilia na kuchanua maua. Kama waridi,

2 litachanua maua, litashangilia sana na kupaza sauti kwa furaha. Litapewa utukufu wa Lebanoni, fahari ya Karmeli na Sharoni; wataona utukufu wa Bwana, fahari ya Mungu wetu.

3 Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea,

4 waambieni wale wenye mioyo ya hofu, “Kuweni hodari, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja, pamoja na malipo ya Mungu, atakuja na kuwaokoa ninyi.”

5 Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa na masikio ya viziwi yatazibuliwa.

6 Ndipo kilema atarukaruka kama kulungu, nao ulimi wa aliye bubu utapaza sauti kwa shangwe. Maji yatatiririka kwa kasi katika nyika, na vijito katika jangwa.

7 Mchanga wa moto utakuwa bwawa la maji, ardhi yenye kiu itabubujika chemchemi. Maskani ya mbweha walikolala hapo awali patamea majani, matete na mafunjo.

8 Nako kutakuwa na njia kuu, nayo itaitwa Njia ya Utakatifu. Wasio safi hawatapita juu yake; itakuwa ya wale watembeao katika Njia ile; yeye asafiriye juu yake, ajapokuwa mjinga, hatapotea.

9 Huko hakutakuwepo na simba, wala mnyama mkali hatapita njia hiyo, wala hawatapatikana humo. Ila waliokombolewa tu ndio watakaopita huko,

10 waliokombolewa na Bwana watarudi. Wataingia Sayuni wakiimba; furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao. Watapata furaha na shangwe; huzuni na majonzi vitakimbia.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0