NENO
🔍 Tafuta katika Biblia

Hosea 14

1 Rudi, ee Israeli, kwa Bwana Mungu wako. Dhambi zako zimekuwa ndilo anguko lako!

2 Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana. Mwambieni: “Samehe dhambi zetu zote na utupokee kwa neema, ili tuweze kutoa matunda yetu kama sadaka za mafahali.

3 Ashuru hawezi kutuokoa, hatutapanda farasi wa vita. Kamwe hatutasema tena ‘Miungu yetu’ kwa kile ambacho mikono yetu wenyewe imetengeneza, kwa kuwa kwako wewe yatima hupata huruma.”

4 “Nitaponya ukaidi wao na kuwapenda kwa hiari yangu, kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao.

5 Nitakuwa kama umande kwa Israeli; atachanua kama yungiyungi. Kama mwerezi wa Lebanoni atashusha mizizi yake chini;

6 matawi yake yatatanda. Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni, harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni.

7 Watu wataishi tena kwenye kivuli chake. Atastawi kama nafaka. Atachanua kama mzabibu, nao umaarufu wake utakuwa kama divai itokayo Lebanoni.

8 Ee Efraimu, nina shughuli gani tena na sanamu? Nitamjibu na kumtunza. Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi; kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu.”

9 Ni nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya. Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa. Njia za Bwana ni adili; wenye haki huenda katika njia hizo, lakini waasi watajikwaa ndani yake.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (Kiswahili Contemporary Version). Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. CC BY-SA 4.0